Tunaposema nyama tunamaanisha misuli iliyopo kwenye mwili wa mnyama ambapo hutumika kama chakula kwa binadamu na hata kwa wanyama wanaokula nyama kama vile Simba, Chui, Mbwa na wanyama wengine wengi tu.
Kwa binadamu nyama tunazokula ni kwa baadhi ya wanyama tu, ingawaje kuna wengine wanakula kila kitu mpaka nyama ya nyoka na pengine hata binadamu wenzao. Pamoja na misuli pia viungo kama maini, moyo, figo, ubongo pia huweza kutumika kama kitoweo kama nyama.
Nyama hapa ulimwenguni huweza kupatikana toka kwenye wanyama kama Ng’ombe, Kondoo, Mbuzi, sungura nk. Hali kadhalika kuna wanyama wa porini kama Nyumbu, Nyati, Swala, Digidigi nk. Mila na desturi pia zinachangia kwenye suala hili la kufanya nyama kuwa kitoweo.
Ni kawaida kwa wanamichezo mbalimbali hapa ulimwenguni mara baada ya kutoka mazoezini au kwenye mashindano kupata chakula ambacho kimeandaliwa vizuri ikiwa ni pamoja na kuwa na kiasi fulani cha nyama kama supu, mboga iliopikwa, kukaangwa, kuokwa na hata nyama choma kama mishikaki au hata mazao ya nyama kama vile soseji,kababu nk.
Nyama na mazao yake ni chanzo muhimu sana cha protini yenye kiwango cha hali ya juu hapa ulimwenguni. Uwepo wa amino acids katika nyama unamchango mkubwa katika kuhakikisha walaji ikiwa ni pamoja na wanamichezo wanapata protini iliyopo kwenye nyama wakati wanapokula vyakula vingine vya jamii ya nafaka, ambavyo hutumika kama vyakula vyao vya kila siku kwenye maeneo wanayoishi.
Nyama inapoliwa huweza kuongeza madini ya chuma ambayo huwa yanafyonzwa kirahisi mno na pia kusaidia ufyonzwaji wa madini hayo ya chuma yaliyopo kwenye vyakula vingine, huku pia ikisaidia ufyonzwaji wa madini ya zinki. Nyama na mazao yake pia ni chanzo muhimu sana cha lile kundi la vitamin B.
Wanamichezo wanapokula nyama na mazao yake huweza kutoa mchango mkubwa sana katika kuondosha matatizo mbalimbali ya lishe kwenye miili yao, ingawa ulaji wa nyama kwa kiasi kikubwa umekuwa ukihusishwa na matatizo ya kiafya kama vile ugonjwa wa gout, kupotea kwa madini ya calcium toka kwenye mifupa, kutokea kwa vijiwe kwenye figo(kidney stones), na kibaya zaidi ni tatizo la ongezeko la mafuta mwilini na lehemu(cholesterol).
Unapokula kiasi kikubwa cha nyama ambayo ndani yake kuna saturated fatty acids hupelekea kupandisha kiwango cha lehemu(cholesterol) kwenye mkondo wa damu na hivyo kujilimbikiza katika mishipa ya damu na kuifanya kuta zake zisinyae kiasi cha kupitisha damu kwa shida zaidi au hata kutopitisha kabisa damu kuelekea kwenye viungo vingine na kupelekea kujitokeza kwa magonjwa ya moyo, mashambulio ya moyo, kiharusi nk.
Maeneo mengi hapa ulimwenguni ambako nyama ndio chakula kikuu, inasemekana karibu robo ya saturated fatty acids huwa inatokea kwenye nyama inayoliwa katika milo mbalimbali iliyo rasmi na isiyo rasmi, na hii imeweza kutumiwa na baadhi ya taasisi kupiga vita ulaji wa nyama hasa nyama nyekundu.
Ingawaje masuala haya ya ulaji nyama kwa kiwango kikubwa yameonekana zaidi katika nchi za magharibi, ambako nyama huweza kuliwa kwa kiasi kikubwa kila siku iendayo kwa Mungu, sambamba na vyakula ambavyo vina kiwango kikubwa cha saturated fatty acids, ikiwa ni pamoja na vile vinavyotengenezwa viwandani, kwenye migahawa na mahoteli makubwa. Huku kwetu kwenye nchi ambazo hazijaendelea, hali ni tofauti kidogo.
Hali kadhalika mbali na ulaji wa nyama kwa kiwango kikubwa pia kuna vitu vingi ambavyo vinahusishwa na magonjwa ya moyo na hata kiharusi, ikiwa ni pamoja na historia ya familia kwa ujumla, uvutaji wa sigara na bangi, madawa ya kulevya, ugonjwa wa kisukari, tabia binafsi ya kupuuzia kufanya mazoezi, shinikizo la damu na hali ya magonjwa mengine.
Kiwango kikubwa cha lehemu(cholesterol) kinatokana na ulaji wa kiwango kikubwa cha nyama hasa yenye mafuta mengi, maziwa na viini vya yai, japokuwa ukivikosa kabisa vyakula hivi unapata matatizo ya lishe duni. Hivyo vyakula hivi vya jamii ya nyama, maziwa na viini vya yai ni vya muhimu sana kwa maisha yetu ya kila siku, kinachotakiwa tusizidishe kiwango cha ulaji wa vyakula hivi. Hasa kwa wale watu ambao wanahisiwa wanaweza kuathirika na ulaji wa vyakula hivyo ambao tayari wana vitambi na unene uliopitiliza.
Kwa kifupi miongozo mingi ya lishe hapa ulimwenguni inapendekeza, kupunguzwa kwa vyakula vinavyochangia kwa kiwango kikubwa cha lehemu(cholesterol) yaani ulaji wake angalau usizidi miligramu 300 kwa siku, huku kiwango kinachoshauriwa kwa siku cha protini inayohitajika mwilini ni gramu 45 hadi 60.
Inafikiriwa kuwa kwa sasa vyakula vyenye mafuta hasa yenye kiwango kikubwa cha lehemu (cholesterol) havina budi kudhibitiwa kwa jamii na wanamichezo ili kujiepusha na magonjwa ya moyo na kiharusi. Maeneo mengine hapa ulimwenguni, miongozo ya lishe inapendekeza kuwa badala ya kula kwa wingi nyama ya ng’ombe ambayo ni nyama nyekundu basi nyama nyeupe kama vile ya kuku,bata na zingine zitumike.
Zipo pia faida za kutokula nyama kwa kiwango kikubwa ikiwa ni pamoja na kurefusha maisha, kuepuka magonjwa ya moyo na kiharusi, kuepuka magonjwa ya kisukari, kansa, kuepuka mashinikizo ya damu,mwili kuwa na uzito sahihi na mwili kuwa na kiwango stahiki cha lehemu(cholesterol).
Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Taasisi ya Afya ya Taifa nchini Marekani, umebaini kuwa watu wanaopenda kula kwa wingi nyama nyekundu, hufa mapema kuliko wale wanaokula kiasi kidogo cha nyama hiyo.
Wapenda nyama ambao wako kwenye hatari kubwa ya kupatwa na saratani na ugonjwa wa moyo ni wale wanaokula kuanzia kiasi cha gramu 112 za nyama (karibu robo kilo) kila siku, lakini wanaokula kiwango kidogo (nusu ya robo kilo) hawako hatarini na badala yake watapata virutubisho muhimu vinavyopatikana kwenye nyama.
Ulaji wa nyama nyekundu wenye faida kwa mwili wa binadamu ni ule unaozingatia kiasi na aina ya nyama. Nyama inayopendekezwa ni steki isiyo na chembe ya mafuta (lean meat) na itakayoliwa kwa kiasi kidogo.
Nyama inahitajika kiafya kwa sababu ina madini ya chuma ambayo ni muhimu kwa wasichana na wanawake wanaotarajia kuzaa. Pia nyama ina Vitamini B12 ambayo husaidia utengenezaji wa DNA na hujenga mishipa na seli za damu. Halikadhalika kuna madini ya zinki ambayo husaidia kuimarisha ufanyaji kazi wa kinga ya mwili. Bila kusahau nyama ina protini ambayo ni muhimu kwa ujenzi wa mifupa na misuli.
Kwa ujumla, nyama nyekundu ni muhimu kwa afya ya binadamu, lakini itakuwa muhimu kama itatumiwa kwa kiwango na kiasi kinachotakiwa. Siku zote wanamichezo waepuke kula nyama yenye mafuta na badala yake wapendelee kula steki isiyokuwa na mafuta ili upate virutubisho vyake muhimu kwa afya yako.
Kula nyama kinyume na mwongozo huu, ni sawa na kuamua kujiweka katika hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo na matatizo mengine ya kiafya, ikiwemo ugonjwa wa miguu au kansa ya tumbo. Tumekuwa tukishuhudia vifo vya ghafla kwa wanamichezo pindi wanapokuwa uwanjani kutokana na matatizo mbalimbali ya moyo ikiwa ni pamoja na mashambulio ya moyo.
Tumeshuhudia pia Fabrice Muamba mchezaji wa timu ya Bolton Wanderers ambae alilazwa katika kituo cha mshituko wa moyo cha London Chest Hospital akiwa katika hali mahututi", kutokana na kuanguka ghafla akiwa mchezoni, hali iliyompelekea astaafu kucheza soka ili kunusuru maisha yake.
Wanamichezo hawanabudi wajiepushe na ulaji wa nyama na vyakula vingine vyote vinavyoweza kupelekea wapatwe na matatizo ya kiafya kwa kiwango kikubwa kwa kuzingatia masharti ya ulaji sahihi. Kama nilivyokwisha sema kuwa nyama ni tamu na muhimu ila tule kwa kiasi ili kuzinusuru afya zetu.
No comments:
Post a Comment