Kutokana na ongezeko la watu duniani ambalo ni tishio kubwa sana inayoweza kuathiri mazingira yetu, si rahisi kuona tena eneo la mazingira asiliya ambalo halijaguswa na binadamu. Sisi sote, mbali na uraia au asili yetu, tumefikwa na changamoto kubwa sana kwa sababu nafasi ya kuishi katika mazingira safi yenye utajiri kiasiliya inazidi kupungua kila siku. Sisi sote tunataka kukaa katika nyumba nzuri, kupata umeme na maji, kuendesha gari na kupanda ndege, kustawisha mimea na kuchuma mazao mengi kushinda mahitaji yetu, na hali kadhalika. Wakati wa kupendelea hivyo, tuna kawaida ya kujiangalia tu kiubinafsi huku tukipuuza viumbe wanaoishi katika mazingira yetu kwa kufikiri kuwa hawana faida. Hilo ni janga kubwa sana ambalo linatukabili sasa kwa sababu mara nyingi tunakosa elimu ya kutosha.
Kwa bahati nzuri, Tanzania bado ina sehemu asiliya ambazo zinaelekea kuwa hifadhi nzuri, lakini tukizingatia hali jinsi ilivyo kwa mtizamo wa juu juu tu. Hususan hifadhi ya Amani, katika safu ya milima ya Usambara ni miongoni mwa misitu ya asili ambayo serikali ya Tanzania imeamua kuitilia maanani kwa sababu ya thamani baioanuai yake kubwa. La kusisitiza kwanza ni kwamba eneo hilo, pamoja na kwamba lina sehemu nyingi za mazingira asiliiya, vile vile lina watu wengi ambao huishi huku tangu zamani. Si la kushangaza basi, hasa katika muktadha hii, kuona kwamba sura ya milima yake ina vipande vipande vya mashamba ya mchai, ambavyo ni tange zinazomilkiwa na watu, pamoja na miti mingine ya kuleta mapato kwa wakaazi wake. Ina maana kwamba maeneo makubwa sana ya asiliya tayari yameshapotea kusudi binadamu aweze kuchuma mazao yake ya kilimo (hasa mchai, mkarafuu, muwa, mdalasini, mahindi na kadhalika). Siyo kwamba wakaazi hawana haki ya kushughulikia shughuli zao za asili (kulima, kukata kuni, kuchuma miti ya porini, na kadhalika), ila msomaji aelewe kwamba binadamu akizidi kukiuka mipaka ya majukumu yake, yaani akizidi kutumia ardhi anakoishi kupita kiasi, athari juu ya mazingira kwa jumla itakuja kuwa ya kiangamizi.
Kwa kifupi, changamoto kwa siku hizi ni hilo : kutunza mali ya watu bila ya kuangamiza yaliyobaki katika mazingira asiliya. Na kutokana na hali hiyo ya utele, utele wa watu, utele wa nyumba, utele wa gari na kadhalika, imekuwa kama kwamba dunia imekuwa finyu zaidi kila kukicha, kiasi cha kukatisha tamaa ya wataalamu ambao wanajitahidi, kila siku, kuwaelimisha watu ili watunze mazingira yao. Kinachobidi sasa ni kujipatia muamuzi mwafaka ambao itakuwa aina ya suluhisho endelevu kwa watu ambao wamebahatika (ingawa hawajajua kwamba ni bahati) kuishi katika mazingira asiliya mithili ya milima ya Usambara. Watu wana haki ya kuzalisha mazao yao ya kilimo lakini pia wanapaswa kukiri kwamba wanyama wadogo kama vile spishi fulani ya ndege au reptilia ambao ni waendemiki wa Usambara wanastahili kuishi na kuwepo kwa enzi zijazo. Je kweli hilo litawezekana wakati tunaambiwa kwamba asilimia 50 ya misitu imeshapotea ?
Wanyama wa msitu
Wanyama wengi huishi katika milima ya Usambara. Katika jamii ya mamalia, eneo la Amani limesharekodi aina 60 ya spishi mbali mbali, kuanzia panya mdogo hadi nguruwe msitu. Mtembezi huenda atakutana na « nyani wa njano » (kg. yellow baboon, kl. Papio cinocephalus), ni rahisi kumkuta kutokana na tabia yake pole sana. Pamoja na nyani huyo, wanyama wengine wanaoonekana kwa wingi ni kama : mbega (kg. Angola pied colobus, kl. Colobus angolensis), kima bluu (kg. Blue monkey, kl. Cercopithecus mitis), nende mwenye miguu mekundu (kg. Zanj sun squirrel, kl. Heliosciurus undulatus), nende wa milimani (kg. Tanganyika mountain squirrel, kl.Paraxerus lucifer), nende wa pwani (kg. red-bellied coast squirrel, kl. Paraxerus palliatus) nende anayepaa (kg. Lord Derby’s Anomalure, kl. Anomalurus derbianus), koni (kg. black and rufous elephant shrew, kl.Rhynchocyon petersi), kuhe (kg. giant pouched rat, kl. Cricetomys gambianus), komba wa Usambara (kg. Usambara galago, kl. Galagoides species)
Ndege adimu
Ndege katika hifadhi ya Amani wako wengi. Wengi hupatikana katika sehemu mbali mbali za Afrika pamoja na nchi nyingine. Wengine ni adimu sana ama wamezoeleka sana kuishi katika milima hii tu. Ina maana kwamba wanapatikana hapa hapa tu duniani, yaani ni ndege au wanyama andemiki. Wengine wameadimika sana kiasi cha kukumbwa na hatari kubwa ya kupotea kabisa. Mmojawapo ni aina ya ndege mwenye mdomo mrefu anayeitwa « kolokolo domo-refu » (kg. Long-billed forest warbler, kl. Artisornis moreaui ) ambaye yupo katika milima ya Usambara ikiwa ni pamoja na sehemu ndogo ya Msumbiji. Kwa hivyo tunapaswa kuwa makini sana katika kuhifadhi mazingira yake endapo tunataka ndege huyo aonekane tena kwa vizazi vijavyo.
Katika takriban aina 350 ya ndege ambao wamerekodiwa katika milima ya Usambara, 12 wako kwenye takwimu ya ndege walioko katika hatari ya kutoweka duniani. Miongoni mwao wapo « bundi wa sokoke » (kg. Sokoke scops-owl, kl. Otus ireneae), « bundi wa Usambara » (kg. Nduk eagle-owl, kl. Bubo vosseleri), « nofi wa Tanzania » (kg. Nicoll’s weaver, kl. Ploceus nicolli), « chozi milia ya kijani », banded green sunbird (kl. Anthhreptes rubritorques), « chozi Amani » (kg. Amani sunbird ; kl. Anthreptes pallidigaster).
Reptilia na viumbe wengine :
Milima ya Usambara imejaaliwa kuwa na karibu jamii 30 za reptilia, wakiwepo vinyonga, nyoka, kenge na mijusi. Takriban jamii 16 za reptilia hazipatikani mahali pengine popote duniani. Miongoni mwao, ndio vinyonga wanaoonekana kwa urahisi sana, hasa usiku. Wako aina mbali mbali, wenye au wasio na pembe, wadogo kwa wakubwa kiasi.
Amphibia kama chura wapo wengi pia. Amphibia hawapungui chini ya spishi 40. Wengi katika hawa ni waendemiki wa milima ya Usambara wala hawapatikani kwingine duniani. Miongoni mwa chura, wasayansi wana kawaida ya kuainisha kila spishi kufuatana na etolojia yake. Hususan chura wa maji (aina ya Xenopus) huishi ndani ya maji tu wala anashindwa kutoka nje. Tofauti na wengine (jamii ya hyperoliidae) ambao huishi juu kileleni kwa miti.
Mwisho katika viumbe hawa wa kiajabu ni vipepeo. Wako wengi sana na mtembezi hawezi kuwakosa katika matembezi yake. Msomaji anaweza kuangalia tovuti hii ifuatayo kuhusu vipepeo wa Tanzania ambao takriban 130 wanapatikana Tanzania pekee wala hawapo nchi nyingine duniani.
Mimea
Zaidi ya aina 3000 za mimea zimeshatambuliwa kwenye milima ya Usambara. Kiasi kinachokadiriwa kuwa asilimia 25 hadi 30 za aina hizi za mimea zinazopatikana katika safu ya milima ya ukanda wa Mashariki, hazipatikani mahali popote duniani. Kati ya hizi nyinginezo zinapatikana Usambara mashariki tu.
Kwa wingi huo wa aina za mimea katika Afrika, mingi yake ikiwa inapatikana hapa tu, Usambara imepewa sifa ya kuwa sehemu mojawapo duniani yenye sifa za pekee iliyorithiwa kutoka kwa vizazi vilivyopita. Ni dhima kubwa ya hifadhi ya Amani kuhifadhi bioanuai hii ya mimea mingi, miongoni mwao ni mingi ya kiajabu au ya kienyeji kama vile :
Mvule (Milicha exelsa) ni aina muhimu sana ya miti inayotumika katika viwanda vya samani. Mivule mingi inaonekana katika mashamba ya chai.
Kihambie (Drypetes usambarica) ni mti wa ajabu inayo maua na matunda yanayokua kwenye shina la mti.
Mhesi (Maesopsis eminii), ni mti ambao umeenea sana katika eneo la Amani ambao matunda yake huliwa na hondohondo. Ndege huyu hutawanya mbegu zake katika msitu ya Amani na kwingineko.
Mkuti (Chrysophyllum perpulchrum) ni mti ambao hutoa matunda yake kuanzia mwezi wa tano (mei) hadi mwezi wa nane (agosti). Majani yake ni mekundu na matunda yana rangi ya kahawia. Matunda yanapendwa na kima na mbegu zake zinaliwa na mpugi wakati zinapodondoka chini.
Mkuyu msitu (Ficus) nao umeenea pia. Huo mti una tabia ya kuota mizizi yake mikubwa sana na hupenda hali ya unyevu kwenye miamba ambayo dughulishi huota juu yake.
Dughulishi (Saintpaulia magungensis) ni aina ya mmea mdogo wenye maua mazuri sana. Hupenda sana mazingira ya msitu wa Amani.
Mzikoziko (Isolona heinsenii) nao hupatikana lakini kwa nadra sana. Upo katika jamii ya mti maarufu sana ambao ni topetope (au mstafeli, Annonaceae). Ni mti ulioadimika sana katika milima ya Usambara. Wenyeji humtumia kwa kujengea.
Mbewe (Tabernae montana) ni aina ya mti mdogo unaopatikana kwa wingi katika eneo la Amani. Majani yake ni makubwa na matunda ya kahawia ni makubwa kama nazi. Imethibitishwa kwamba matunda yake yanatumika kutibu matatizo ya moyo na figo yanapochanganywa na mimea ya aina nyingine.
Miti mingi mengine ambao ni muhimu ipo kama vile msambo (Allanblackia stuhimannii) ambao mbegu zake huwapatia weneyji mafuta ya kupikia. Mpumu (Anthocleista grandiflora) nao ni mti maarufu pia kwa kuwa na majani mapana sana. Unajulikana kwa kupatikana kwa dawa ya pumu (asthma). Long’we (Cyathea manniana)ni mti pia ambao magome yake hutibu matatizo ya tumbo. Ng’oko (Piper capense) unaota mzizi ambao unatumika katika kujenga nguvu za kiume. Ng’waka (Annickia kummeriae) pia huota magome ambayo huchangia katika kutibu malaria na vidonda.
Kama unataka kuchunguza na kujua zaidi, hii ifuatayo ni tovuti nzuri sana :
No comments:
Post a Comment