MAWAZO YA KILA MWANAFAMILIA YAHESHIMIWE
Katika kipindi kigumu cha maisha ni rahisi sana kukumbwa na udikteta wa mawazo kiasi cha kuamini kuwa, hakuna anayeweza kuleta mawazo sahihi ya kukabili changamoto zaidi yako wewe kiongozi.
Katika hali ya kawaida, wakati huu ndiyo mbaya zaidi kwenye upofu wa maamuzi kwa sababu akili huchoshwa na msongo mkali wa mawazo jambo linaloweza kuzalisha haraka uamuzi usiofaa.
Ukiwa kama kiongozi wa familia na uko kwenye msoto wa maisha na giza la hali ngumu limezidi kutanda, ni vema kuwashirikisha wanafamilia wote, mjadili namna ya kupambana na dhiki na ikiwezekana mawazo ya kila mmoja yazingatiwe bila kujali huyu ni mwanamke au mtoto.
JENGA HALI YA KUAMINIANA
Kuna baadhi ya viongozi wa familia duni ambao wakati wa dhiki ndiyo huongeza kasi ya kulewa wakijitetea kuwa, wanapoteza mawazo kwa pombe za ofa.
Ukweli ni kwamba, familia inaweza isikuamini kama kweli unakwenda baa au klabuni kununuliwa pombe kila siku, badala yake itakuona kama unafuja kinachopatikana kwa ulevi na kwamba umeitelekeza familia yako.
Kiongozi wa familia lazima ajenge hali ya kuaminiana kwa kila mtu, isiwe hawa wanalala njaa, mwingine anaonekana na nguo mpya.
FURAHIA USHINDI HATA MDOGO
Ikiwa familia imepambana na kupata sehemu ndogo ya mafanikio, kiongozi anatakiwa kufurahia ushindi huo na wapiganaji wenzake ndani ya familia, iwe kwa kununua kuku na kupiga wali ‘spesho’ au kununuliana nguo mpya kwa lengo la kujipongeza kwa mafanikio.
Kitendo hiki hutia moyo watendakazi na kuwafanya waongeze bidii wakiamini kupata kuna faida ya kila mtu. Kamwe kiongozi asiungane na familia yake kwenye shida tu halafu sehemu ya mafanikio ikipatikana ajitenge na kwenda kutumia na watu wengine kwenye nyumba za starehe, jambo hili huvunja moyo sana.
KINGA MIGAWANYIKO
Familia duni haipaswi kugawanyika kwa namna yoyote. Wazazi wengi wamekuwa na tabia ya kuzigawa familia kimatabaka au ulevi wa kupenda. Utakuta watoto wawili wanampenda zaidi baba kuliko mama na hawa wanamuunga mkono mama zaidi ya baba kwa sababu za kipuuzi.
Kiongozi wa familia hatakiwi kuendekeza usaliti kwenye familia bali kujenga umoja na usawa usiokuwa na mgawanyiko ili kuleta tija katika vita ya kujikomboa kimaisha.
THAMINI MCHANGO WA KILA MTU
Kila mtu anavyochangia pato kwenye familia anatakiwa kuheshimiwa bila kuangalia kiasi. Endapo mtoto mkubwa ni mbeba zege na huchangia shilingi 1,000 kila siku basi aheshimiwe na kutiwa moyo.
Viongozi wengi wa familia hasa wazazi wamekuwa na desturi ya kuwapenda zaidi watoto au ndugu wanaochangia pato kubwa na kuwadharau wale wanaoleta fedha kidogo au kuhudumia familia kwa hali zao peke yake. Hilo si jambo zuri.
No comments:
Post a Comment